1 Corinthians 14

Karama Za Unabii Na Lugha

1 aFuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii. 2 bKwa maana mtu yeyote anayesema kwa lugha, hasemi na wanadamu bali anasema na Mungu. Kwa kuwa hakuna mtu yeyote anayemwelewa, kwani anasema mambo ya siri kwa roho. 3 cLakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji. 4 dAnenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii hulijenga kanisa. 5 eNingependa kila mmoja wenu anene kwa lugha lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa atafsiri, ili kanisa lipate kujengwa.

6 fSasa ndugu zangu, kama nikija kwenu nikasema kwa lugha mpya nitawafaidia nini kama sikuwaletea ufunuo au neno la maarifa au unabii au mafundisho? 7Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, kama vile filimbi au kinubi, mtu atajuaje ni wimbo gani unaoimbwa kusipokuwa na tofauti ya upigaji? 8 gTena kama tarumbeta haitoi sauti inayoeleweka, ni nani atakayejiandaa kwa ajili ya vita? 9Vivyo hivyo na ninyi, kama mkinena maneno yasiyoeleweka katika akili, mtu atajuaje mnalosema? Kwa maana mtakuwa mnasema hewani tu. 10Bila shaka ziko sauti nyingi ulimwenguni, wala hakuna isiyo na maana. 11 hBasi kama sielewi maana ya hiyo sauti, nitakuwa mgeni kwa yule msemaji, naye atakuwa mgeni kwangu. 12 iVivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani kuwa na karama za rohoni, jitahidini kuzidi sana katika karama kwa ajili ya kulijenga kanisa.

13 jKwa sababu hii, yeye anenaye kwa lugha na aombe kwamba apate kutafsiri kile anachonena. 14 kKwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haina matunda. 15 lNifanyeje basi? Nitaomba kwa roho, na pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho na nitaimba kwa akili yangu pia. 16 mIkiwa unabariki kwa roho, mtu mwingine atakayejikuta miongoni mwa hao wasiojua, atawezaje kusema “Amen” katika kushukuru kwako, wakati haelewi unachosema? 17 nMnaweza kuwa mnatoa shukrani kweli, sawa, lakini huyo mtu mwingine hajengeki.

18Namshukuru Mungu kwamba mimi nanena kwa lugha kuliko ninyi nyote. 19 oLakini ndani ya kanisa ni afadhali niseme maneno matano ya kueleweka ili niwafundishe wengine kuliko kusema maneno 10,000 kwa lugha.

20 pNdugu zangu, msiwe kama watoto katika kufikiri kwenu, afadhali kuhusu uovu mwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri kwenu, mwe watu wazima. 21 qKatika Sheria imeandikwa kwamba: “Kupitia kwa watu wenye lugha ng’eni
na kupitia midomo ya wageni,
nitasema na watu hawa,
lakini hata hivyo hawatanisikiliza,”
asema Bwana.

22 rBasi kunena kwa lugha ni ishara, si kwa watu waaminio, bali kwa wasioamini, wakati unabii si kwa ajili ya wasioamini, bali kwa ajili ya waaminio. 23 sKwa hiyo kama kanisa lote likikutana na kila mmoja akanena kwa lugha, kisha wakaingia wageni wasioelewa wasioamini, je, hawatasema kwamba wote mna wazimu? 24 tLakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote, 25 unazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko katikati yenu!”

Kumwabudu Mungu Kwa Utaratibu

26 vBasi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kanisa. 27Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri. 28Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.

29 wManabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo. 30 xKama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze. 31Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo. 32 yRoho za manabii huwatii manabii. 33 zKwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani.

Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu,
34 aawanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo. 35 abKama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lolote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani.

36 acJe, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia? 37 adKama mtu yeyote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana. 38Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.

39 aeKwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha. 40 afLakini kila kitu kitendeke kwa heshima na kwa utaratibu.
Copyright information for SwhKC